Kesi ya SCORPION Yapigwa Kalenda
Upande wa Jamhuri kwenye kesi ya Salim Njwete maarufu kama 'Scorpion' anayetuhumiwa kumwibia Saidi Mrisho na kumtoboa macho kwa kisu umedai mahakamani hapo kwamba upelelezi haujakamilika na kuomba siku nyingine ya kukamilisha.
Mshitakiwa Njwete 34, anashitakiwa kwa kumwibia Mrisho na kumjeruhi kwa kumchoma tumboni, mabegani na machoni.
Taarifa ya upelelezi kutokamilika ilielezwa jana na Mwendesha Mashitaka Chensensi Gavyole mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule kesi hiyo ilipotajwa na kuangaliwa kama upelelezi umekamilika.
“Mshitakiwa yuko mbele ya Mahakama hii lakini upelelezi haujakamilika, tunaomba Mahakama itupangie siku nyingine ya kutajwa kutokana na upelelezi kuendelea,” alisema Gavyole.
Kutokana na sababu hizo, Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 16 itakapotajwa tena.
Mshitakiwa huyo maarufu kama Scorpion alifikishwa mahakamani hapo akiwa kwenye gari dogo la mizigo tofauti na siku za nyuma ambapo alikuwa akiletwa akiwa kwenye basi la Magereza.
Awali ilidaiwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 9 Buguruni Sheli alipomwibia Mrisho fedha na vitu vyenye thamani ya Sh 476,000 na kumjeruhi kwa kumchoma kisu tumboni, mabegani na machoni.
No comments:
Post a Comment