Shinzo Abe: Nina imani na Donald Trump
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema ana imani na Rais Mteule wa Marekani Donald Trump na kwamba wawili hao wanaweza kuaminiana.
Bw Abe ameeleza mkutano wa dakika 90 kati yake na Bw Trump katika jumba la Trump Tower, New York, kama wa uwazi na wa kirafiki.
Wakati wa kampeni, Bw Trump alitilia shaka manufaa ya urafiki kati ya Marekani na baadhi ya washirika wake wa muda mrefu, ikiwemo Japan.
Mkutano huo ulikuwa wa kwanza wa ana kwa ana kati ya Trump na kiongozi wa nchi nyingine duniani tangu ashinde urais.
Marekani na Japan zimekuwa washirika wakubwa tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ambapo Marekani iliisaidia Japan kufufua tena uchumi wake.
- Familia ya Donald Trump: Wake na watoto
- Uongozi wa Trump: Maswali na majibu
- Hillary Clinton aenda kutembea porini
Trump ameahidi kufuta mktaba wa kibiashara kati ya Marekani na nchi za Pasifiki, ambapo Bw Abe amekuwa wakiuunga mkono sana kama njia ya kukabili ubabe wa kiuchumi wa China.
Mkataba huo uliidhinishwa na bunge la Japan, licha ya uwezekano kwamba huenda ukafutwa Bw Trump atakapoingia madarakani.
Bw Trump pia alisema Japan inafaa kulipia zaidi kwa ajili ya wanajeshi wa Marekani walio kwenye ardhi ya Japan kutoa ulinzi.
Aidha, ametoa pendekezo la Japan na Korea Kusini kustawisha silaha za nyuklia kukabili tishio kutoka kwa Korea Kaskazini.
Mkutano huo inadaiwa ulipangwa baada ya Bw Abe kumpigiakura Trump kumpongeza kwa kushinda uchaguzi wa urais, na kisha akamtajia kwamba angepitia New York akielekea Peru kuhudhuria mkutano wa kibiashara kati ya Asia na nchi za Pasifiki.
Akiongea baada ya mkutano huo, Bw Abe alisema: "Tulikuwa na mazungumzo ya kirafiki na ya kufana sana kwa kipindi kirefu. Yalikuwa mazingira ya kirafiki.
"Ninaamini kwamba bila kuaminiana kati ya nchi hizi mbili ushirikiano wetu hauwezi kufanya kazi siku zijazo na kama matokeo ya mazungumzo yetu leo, nimeshawishika kwamba Bw Trump ni kiongozi ambaye ninaweza kuwa na imani sana naye.
Kiongozi uyo wa Japan hakutoa maelezo mengi kuhusu mkutano huo lakini alisema watakutana tena kujadili kwa kina baadhi ya masuala muhimu.
Katika siku chache baada ya ushindi wake, Bw Trump amezungumza na viongozi kadha wa nchi mbalimbali kwa simu pamoja na baadhi ya watu anaotarajiwa kuwateua kuwa mawaziri katika jumba la Trump Tower.
Mengine yaliyotokea:
- Luteni Jenerali Mstaafu Michael Flynn amepewa kazi ya kuwa mshauri mkuu wa usalama wa taifa, vyombo vya habari Marekani vimeripoti.
- Waliomtembelea Trump Tower Alhamisi ni pamoja na waziri wa mambo ya nje wa zamani Henry Kissinger na gavana wa South Carolina Nikki Haley, mmoja wa wanaotarajiwa kupewa kazi ya waziri wa mambo ya nje
- Mgombea urais wa zamani wa chama cha Republican Mitt Romney atakutana na Bw Trump wikendi hii, kwa mujibu wa vyombo vya habari Marekani
- Bw Trump atazru majimbo ambayo alishinda kwa mikutano ya kusherehekea ushindi kwa mujibu wa mkurugenzi wake wa kampeni George Gigicos
Kwingineko, makamu wa rais mteule Mike Pence, ambaye pia anaongoza kundi la mpito la Bw Trump amesema ana imani utawala wa Trump utafanya kazi na wafuasi wa chama cha Democratic.
Hayo yakijiri, Rais Barack Obama amemhimiza mrithi wake kuikabili Urusi iwapo itakiuka maadili na sheria za kimataifa.
Baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin, Bw Obama amesema anatumai Bw Trump hatakuwa tu mtu wa kucheza siasa na maneno matupu na Urusi.
No comments:
Post a Comment