Kampuni ambayo huanza kazi saa 3.06
Si kampuni nyingi duniani ambazo husisitiza wafanyakazi wake waanze kazi muda usio wa kawaida kama kampuni ya Pivotal Software nchini Marekani.
Wafanyakazi katika kampuni hiyo ya Marekani yenye afisi 20 maeneo mbalimbali duniani hutakiwa kuwa tayari na kuanza kazi inapogonga saa tatu na dakika sita kila asubuhi.
Wakati huo kengele hulia na wafanyakazi wote hukusanyika kwa mkutano mfupi ambao hudumu kati ya dakika tano na dakika 10.
Kisha, wataalamu hao wa programu za kompyuta huketi kwenye mashine zao na kuanza kuchapa kazi. Huwa hakuna mikutano mingine baada ya hapo wala mambo mengine ya kuwasumbua.
Mwanzilishi wa Pivotal, ambayo husaidia kampuni nyingine kujiboresha katika kuandika programu za kompyuta, Bw Rob Mee, ambaye pia ni afisa mkuu mtendaji, anasema hilo linatokana na haja na kuwawezesha wafanya kazi kufanya kazi nzuri ya uzalishaji.
"Niligundua kwamba wataalamu wa programu za kompyuta, ukiwaacha wenyewe wajitawale, wanaweza wakaingia hata saa nne asubuhi," anasema.
"Na iwapo hawajala, watakuwa wanahisi njaa kufikia saa tano, kwa hivyo wataanza kutafuta chakula, na hili litafanya adhuhuri yao kuwa ndefu. Hivyo hawatafanya kazi vyema.
"Kwa hivyo, tulifikiria, 'tumpatie kila mtu kiamsha kinywa.' Na hili huwapa sababu ya kufika mapema."
Wafanyakazi wote katika kampuni hiyo hupewa staftafi bila malipo kila asubuhi kabla ya kazi kuanza.
Lakini mbona iwe saa 3.06 asubuhi na si wakati mwingine?
"Tulidhani kwamba tukisema ni saa 3, wataalamu hawa wa kompyuta wanapojichangamsha kuhusu kazi ya siku, wanasema kusema 'kama ni saa tatu, nitachelewa kidogo'," anasema Be Mee.
"Lakini tukafikiria, 'mbona tusiweke saa 3.05 asubuhi', lakini hapo tungekuwa tumeeleza kwa ufasaha zaidi, na kwa sababu wataalamu wa programu za kompyuta huwa hawapendi kutumainia mema sana, tulichaguasaa 3.06. Baada ya hapo, watu walianza kufurahia."
Wakati wa kuanza, na kumaliza kazi
Kazi hufungwa saa kumi na mbili jioni na kila mfanyakazi hutakiwa kuondoka afisini.
Hakuna anayekubaliwa kufanya kazi ya ziada.
Bw Mee anasema: "Wataalamu wa programu za kompyuta huwa hawafanyi kazi vyema iwapo wamechoka sana, kwa hivyo huwa hatuwakubali kufanya kazi hadi usiku."
Ingawa mtazamo wa Pivotal kuhusu watu kufika kazini kwa wakati asubuhi huenda ukaonekana wa kushangaza, kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni zilizofanikiwa sana.
Kampuni hiyo inakabiliwa kuwa na thamani ya $2.8bn (£2.4bn), ina kampuni zilizowekeza katika hisa za kampuni hiyo ni pamoja na Dell Technologies, Microsoft, General Electric, na kampuni ya magari ya Ford.
Wataalamu wa kampuni ya Pivotal, husaidia kampuni nyingine kujiboresha katika kuandika programu za kompyta.
Wateja wa kampuni hiyo ni pamoja na BMW, Mercedes-Benz, Lockheed Martin, NBC, Bloomberg, Orange, eBay, South West Airlines, na Twitter.
Hata Google waliomba usaidizi wa Pivotal nyakati za mwanzo.
Kampuni hiyo ya Bw Mee pia husaidia kampuni za kukusanya habari za kijasusi.
Wafanyakazi wa kampuni zinazosaidiwa na Pivotal huungana na mfanyakazi wa Pivotal na kuandika programu ya kompyuta kwa pamoja.
Bw Mee alisomea Chuo Kikuu cha California, Berkeley. Alifanya utafiti nchini Japan miezi mitatu katika kampuni ya IBM kabla ya kurejea Marekani na kuwa mshauri huru kuhusu masuala ya kompyuta.
Alianzisha Pivotal, mwanzo akiiita Pivotal Labs, mwaka 1989, akitumia jina lililopendekezwa na mamake.
Bw Mee alimiliki kampuni hiyo hadi 2012 alipouza biashara hiyo kwa EMC lakini akasalia kama afisa mkuu mtendaji.
No comments:
Post a Comment