Lugora: Mawaziri acheni kumpotosha Rais
MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) amewaonya baadhi ya mawaziri kutompotosha Rais John Magufuli kuwa fedha zimepotea, kutokana na baadhi ya watu kuficha majumbani kwenye magodoro wakati hiyo si sababu.
Sambamba na hilo, amewaonya wabunge wa upinzani, kuacha kuwatumia vibaya wananchi na kuwachonganisha na Rais wao, baada ya kuona wamebanwa kulipa kodi.
Mbunge huyo alitoa onyo hilo jana wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/2018 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
“Nyinyi mawaziri ni abiria na mmekaa siti za mbele kwenye gari analoendesha Rais Magufuli msimkimbize, baadhi yenu msimpotoshe rais yeye si mchumi mtamletea matatizo mbeleni, pesa zimepotea si kwa sababu zimefichwa kwenye magodoro ila zimepotea kwa sababu pesa zote zimewekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zitoeni pesa hizo ziende kwenye mabenki,” alisema.
Alisema Bunge limepoteza mwelekeo, limekuwa la kulialia na kumlaumu Rais Magufuli kwa sababu amebana wakwepa kodi na kufafanua “Rais aliliomba Bunge hili limsaidie kutumbua majibu, tumsaidie mipango ya serikali iweze kutekelezeka ili kujenga nchi yetu, najua Rais ana nia njema na nchi, Hapa Kazi Tu inawafanya wafanyabiashara waliozoea kukwepa kodi wamebanwa sasa wanalia biashara imekufa, watumishi waliozoea posho za hapa na pale, kusafiri wamebanwa, wabunge tuliozoea kula andazi la inchi 18 sasa tunakula la sentimita mbili, kwenye kamati tumebanwa posho, tunalialia kisa tumeshikwa pabaya na kuwaingiza wananchi wanyonge eti hawana pesa.
"Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe umepewa gari na serikali na mafuta unawekewa, yamejaa kwenye gari, kiyoyozi kipo saa 24 unasema serikali imefilisika huku unawachonganisha wananchi na Rais wao, unawatumia vibaya wananchi, Msigwa kama Mchungaji (Peter, Mbunge wa Iringa Mjini) tumia taaluma yako kuwashauri wenzako wawe kwenye safari hii... Rais Magufuli anatupeleka Kaanani kuishi maisha mazuri, ametupandisha basi kutupeleka nchi ya ahadi.
"Nashauri anapoendesha gari ajue kuna matuta, akiendesha vibaya Watanzania atatuangusha, kuna zebra na wanafunzi wanavuka, akiona spidi iko 50 apunguze mwendo... na nyinyi mawaziri mmekaa siti za mbele za gari la Rais, msimpotoshe”, alifafanua.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde(CCM) alisema ni lazima uchumi unapokua, uoneshe kwenye maisha ya wananchi wa vijijini ; na si kuonesha ujuaji wa pointi kwenye makaratasi.
Alisema “Upinzani msizunguke kusema serikali imefilisika, semeni ukweli, Mbowe umefilisika, umeshindwa kulipa madeni, serikali haijafilisika, inalipa mishahara, inalipa madeni yake”.
Naye Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema kila sehemu kuna njaa, mtaani wananchi wanalia hakuna pesa na hata wabunge wamepauka kwa kukosa fedha.
No comments:
Post a Comment