Kenya yaahirisha kufunga kambi ya Dadaab
Serikali ya Kenya imeahirisha uhamisho wa wakimbizi wa Kisomalia kwa miezi sita ili kuruhusu majadiliano na ufadhili.
Hatahivyo, waziri wa maswala ya ndani Jenarali Joseph Nkaissery amesema kuwa uhamisho wa kujitolea kwa takriban watu 280,000 katika kambi hiyo kubwa duniani Dadaab utaendelea.
Tangazo hilo linajiri siku moja baada ya makundi ya haki za kibinaadamu kushtumu serikali kwa kuwalazimu wakimbizi kurudi nyumbani licha ya hali ngumu katika taifa lao.
Serikali imetangaza mipango ya kufunga kambi hiyo kufikia mwisho wa mwezi huu.
Jenerali Nkaissery amesema kuwa uhamisho wa wakimbizi hao utafanyika kwa njia ya kibinaadamu na yenye heshima,kufuatia madai kutoka kwa makundi ya kupigania haki za kibinaadamu kwamba serikali ya Kenya imekuwa ikiwalazimisha wakimbizi hao kuondoka.
Kenya imeweka mpango wa mwezi hadi mwezi ambao unashirikisha kusitisha usajili wa mara mbili wa wakimbizi hao kama raia wa Kenya, kuwahamisha wakimbizi wasio raia wa Somalia hadi kambi nyengine, kuwahamisha wakimbizi wa Somalia hadi mataifa mengine na hatimaye kuifunga kambi ya Dadaab.
No comments:
Post a Comment