Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm, amesema pamoja na kupoteza michezo miwili kwenye ligi ya Vodacom, lakini bado wanayo nafasi ya kutetea ubingwa wao msimu huu.
Pluijm ameiambia Goal, baada ya kupoteza mchezo uliopita mikakati yao hivi sasa ni kuhakikisha hawarudii tena makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo na Mbeya City hadi kupoteza.
“Haikuwa matarajio yetu lakini ndiyo imeshatokea japo ilikuwa ni lazima tufungwe kwa mazingira yaliyokuwepo lakini pamoja na yote bado Yanga inayo nafasi ya kutetea ubingwa wake kwasababu kuwa nyuma kwa pointi nane sidhani kama nikikwazo kwetu,”amesema Pluijm.
Mdachi huyo  amesema hali kama hiyo siyo mara ya kwanza kuikumba Yanga, katika misimu iliyopita lakini waliweza kutoka nyuma na kubeba ubingwa na hilo linawezekana kutokea msimu huu kwani bado ana kikosi imara.
Anasema anajua kama watani zao wa jadi Simba wamekuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi ya msimu huu, lakini hilo halimfanyi yeye kuwa na hofu na kupoteza matumaini ya kufanya vizuri kwenye mechi zao.
“Tumesahau yaliyopita na sasa tumeelekeza nguvu zetu kwenye mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons ni mchezo mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi ili kupunguza presha kwa mashabiki wetu lakini pia kuwanyima raha wapinzani wetu Simba wanaoongoza ligi,” alisema Pluijm.
Pluijm amesema mafanikio waliyoyapata msimu uliopita yamekuwa kama sababu ya kukamiwa na timu nyingi wanazocheza nazo na kila moja wapo ikitaka kuwafuwanga.
Amesema anawapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kupambana na kupigania ushindi kwa timu yao licha ya kuwepo kwa vikwazo vingi vya kuwakatisha tamaa kutoka kwa baadhi ya watu.
“Wapo watu wamekuwa wakituponda na kutukatisha tamaa kwa kusema Yanga ni timu ambayo inapendelewa jambo ambalo halina ukweli na walitakiwa wakubaliane na mabadiliko ya soka na kuwapa pongezi wachezaji wangu kwa kazi wanayoifanya kama tungekuwa tunapendelewa tusingeweza kuwa mabingwa mara mbili mfululizo na kubeba kombe la FA na wachezaji wetu kubeba tuzo mbalimbali kutoka kwa wadhamini wa ligi ya Vodacom.