Rais Magufuli Aishauri Benki ya Dunia kutoa Mikopo kwa wakati unaofaa ili utekelezaji wa miradi ufanyike kwa haraka.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Novemba, 2016 amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na kuzungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani Bilioni 1.6 zikiwa ni mkopo kutoka benki hiyo.
Akizungumza baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi. Bella Bird amesema mikopo hiyo inalenga kusaidia juhudi za maendeleo nchini Tanzania na itatolewa katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati, usafirishaji, elimu na maji.
"Miradi hii yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika maisha ya Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na msukumo mzuri kutoka Serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia maendeleo" amesema Bi. Bella Bird.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi.
"Tunataka kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi hii ina manufaa makubwa kwa watanzania na tungependa utekelezaji wake ufanyike haraka, na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa"amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa sasa na itakayoanza kutekelezwa katika siku zijazo kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kwa hivi sasa miradi 26 yenye thamani ya Jumla ya Dola za Marekani Bilioni 4.5 inatekelezwa hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment